BEKI wa Inter Milan Miranda ndie amepewa Utepe wa Kepteni wa
Brazil wakati Ijumaa Alfajiri ikicheza Ugenini huko Mjini Montevideo na Uruguay
katika Mechi ya Kundi lao la Nchi za Marekani ya Kusini ya kusaka Washiriki wa
Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.
Baada ya Kepteni wa Brazil Neymar kujiuzulu wadhifa huo Julai
Mwaka Jana na tangu ashike madaraka Juni 2016 Kocha wa Brazil Tite alisema
atakuwa hana Nahodha wa kudumu na badala yake kuuzungusha Utepe wa Kepteni
miongoni mwa Wachezaji vingunge wa Kikosi chake.
Miranda ndie alikuwa Kepteni wa kwanza wa Kikosi cha kwanza kabisa
cha Tite Brazil ilipoichapa Ecuador 3-0 huko Quito Septemba 2016.
Wengine waliowahi kuuvaa Utepe huo ni Dani Alves mara
2 (dhidi ya Colombia na Argentina), Fernandinho (Peru), Filipe Luis
(Venezuela) na Renato Augusto (Bolivia) zote zikiwa Mechi za Kundi lao za Kombe
la Dunia 2018.
Pia, Robinho na Diego walikuwa ndio Manahodha Brazil ilipocheza
Kirafiki na Colombia Mwezi Januari kwenye Mechi ambayo Kikosi cha Tite kiliundwa
na Wachezaji waliokuwa wakicheza ndani Nchini Brazil pekee.