LEO huko Goodison Park Jijini Liverpool ipo Dabi ya Kitongoji cha Merseyside kati ya Mahasimu Everton na Liverpool ambayo Mashabiki wanangoja kujua nani atapewa furaha ya mapema ya Sikukuu ya Krismasi.
Hii ni Mechi ya EPL, Ligi Kuu England na inazikutanisha Liverpool iliyo Nafasi ya 3 na Everton walio Nafasi ya 9.
Ushindi kwa Liverpool utawakweza hadi Nafasi ya Pili na kuwa Pointi 6 nyuma ya Vinara Chelsea na Pointi 1 mbele ya City.
Ikiwa Everton watashinda basi watapanda hadi Nafasi ya 7.
Liverpool na Everton zinatinga kwenye Mechi hii wakitoka kwenye ushindi Mechi zao za mwisho za EPL ambapo Liverpool iliinyuka ugenini Watford 3-0 na Everton kushinda kwao Goodison Park kwa kuichapa Arsenal 2-1.
Lakini Uwanjani Goodison Park, Everton na Liverpool zimetoka Sare 4 katika Mechi zao zilizopita na mara ya mwisho kwa Everton kushinda kwao ni Mwaka 2010 waliposhinda 2-0.
The Capital Tz.Com tunakuunganisha na Abbas Pira mtanzania aliyeko nchini England kuuchambua mchezo huo kwa sauti.