Leo
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt John Pombe Magufuli
ameongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kilichofanyika
katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kikao
hiki kilikuwa ni kikao chake cha kwanza tangu alipokabidhiwa mikoba ya
kukiongoza cha hicho baada ya mwenyekiti aliyekuwepo Dkt Jakaya Mrisho
Kikwete kuomba kung’atuka kabla ya muda wake kuisha.
Akizungumza
na wajumbe wa NEC leo, Dkt Magufuli ametaja mambo 10 ambayo anaanza
nayo kama mwenyekiti wa CCM. Mambo hayo na haya yafuatayo;-
1. Rushwa
Mwenyekiti
wa CCM Dkt Magufuli alisema kuwa chama hicho ni miongoni mwa taasisi
zinazotuhumiwa sana kwa uwepo wa mianya ya rushwa hasa kipindi cha
uchaguzi ndani ya chama au serikali. Amesema katika kipindi chake cha
uongozi atahakikisha hakuna kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa.
2. Uimarishaji wa chama
Jambo
la pili alilosema wakati akizungumza na wajumbe wa NEC zaidi ya 370
alisema kuwa ni kujenga chama imara kitakachoweza kuwatetea wananchi na
kulinda rasilimali zao. Dkt Magufuli alisema wao wamechaguliwa na
wananchi kupitia chama hivyo hawapaswi kuwa sehemu ya walalamikaji.
3. Wanachama
Chama
ni wanachama, ndivyo alivyosema akielezea kuwa ni lazima chama
kihakikishe kinaongeza udadi ya wanachama wake hasa vijana. Aidha,
ametahadharisha kuwa wanachama hao wasiwe wananchama hewa, bali wawe ni
wanachama wakukitumikia chama na watakaolipa ada.
4. Chama kujitegemea kiuchumi
CCM
ina vitega uchumi vingi sana, lakini kila mara tunakuwa ni ombaomba
hasa kipindi cha uchaguzi. Katika kipindi changu cha uongozi hili sitaki
kuliona. Ni lazima tuhakikishe mali za chama zinakinufaisha chama na
tuweze kujitegemea bila kuwa tegemezi kwa mtu yeyote, alisema mwenyekiti
Dkt Magufuli.
5. Wasaliti na makundi
Kumekuwepo
wanachama ambao si waaminifu ndani ya chama, hawa ni hatari ni lazima
tuhakikishe tunakuwa na wanachama wakweli. Pia akizungumzia suala la
makundi Dkt Magufuli alisema kuwa makundi ndani ya chama hasa wakati wa
uchaguzi yamezidi kushamiri, na wengi huendeleza makundi hata baada ya
uchaguzi, ni wakati wa kujenga CCM mmoja.
6. Chama Imara kuanzia chini
Hapa
alieleza kuwa chama imara ni kile chenye mizizi kuanzia ngazi za chini.
Ni lazima tuwe na chama imara kuanzia ngazi za shina, tawi, kata,
wilaya, mkoa hadi taifa. Hili litafanukiwa kwa sisi tulipo huku juu
kushuka hadi chini katika jitihada za kueleza sera zetu kwa wananchi.
7. Nafasi za uongozi
Mwenyekiti
wa CCM amesema kuwa wakati wa mtu kuvaa kofia nyingi ndani ya chama
ufike mwisho na kuwa sasa ni wakati wa nafasi moja ya uongozi kushikwa
na mtu mmoja. Akifafanua hili alisema kuwa litasaidia kutoa nafasi kwa
watu wengine pia kukitumikia chama.
8. Kufutwa vyeo
Akielezea
katiba ya CCM, Dkt Magufuli alisema kuwa katika awamu yake ya uongozi
anataka vyeo ambavyo havujatajwa kwenye katiba ya chama visiwepo. Akitoa
mfano wa vyeo hivyo alisema ni pamoja na Jumuita ya Wazazi, Chipukizi.
9. Uwajibikaji
Alisema
kuwa chama kina wajibu wa kuwatumikia wanachama wote bila ubaguzi.
Alisisitiza kuwa katika awamu yake ya uongozi hatokubali kuona watu
wachache wa vyeo vya juu wananufaika na chama na mamia ya wanachama wa
chini wakiteseka.
10. Nguvu ya chama
Jambo
hili ambalo alilisema kwa msisitizo na hata kulirudia mara mbilia ni
kuwa, anataka chama kinachoongoza wananchama na si wananchama au
mwananchama anyeongoza chama. Akitilia mkazo hapa alisema mwanachama
ndiye anapaswa kukifuata chama na si chama kumfuata mwanachama au
wanachama wachache.