Na.
Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar
es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki
amewaagiza viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa
wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani
wakazi wa jiji la Dar es salaam wanaovunja sheriaza jiji kwa
kuendesha shughuli mbalimbali katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Aidha
amewataka waendesha pikipiki maarufu kwa jina la “Bodaboda”, Bajaji,
waendesha baiskeli na mikokoteni wanaofanya biashara ya kubeba abiria na mizigo
maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kuondoka wenyewe kabla hatua kali za kisheria
hazijachuliwa dhidi yao.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Saidi Mecki Sadiki amesema kuwa jiji la Dar es salaam limeamua kuchuakua
uamuzi huo kufuatia tatizo la baadhi ya wananchi kuamua kuvunja sheria
zilizowekwa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na kutafuta fedha hali inayoleta
usumbufu kwa wananchi wengine .
Amesema
kuwa licha ya changamoto inayolikabili jiji la Dar es salaam hasa maeneo ya
katikati ya mji hali iliyopo sasa ya biashara holela na uvunjifu wa sheria
unaofanywa na maendesha Bodaboda, Bajaji, baiskeli, mikokoteni na Taxi bubu
maeneo yasiyoruhusiwa kisheria hauwezi kuvumilika.
“Jiji
la Dar es salaam tumekuwa na kero ya muda mrefu hasa ya omba omba, waendesha
baiskeli, bodaboda na wafanyabiashara katika maeneo ya makutano ya barabara
katika maeneo yasiyoruhusiwa hali hii hatuwezi kuivulimia, sisi hatufukuzi watu
bali tunawataka wafuate sheria za jiji” Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa serikali haina lengo la kuwazuia wananchi kufanya biashara na shughuli
nyingine za kujiingizia vipato kama wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa
na kuongeza kuwa wale wote wanaoomba leseni za kufanyia biashara wanapewa
taratibu na miongozo na masharti ya kuzingatia wanapofanya biashara zao jambo
ambalo wengi wao wanashindwa kulizingatia.
“Kila
Manispaa ina miongozo na kanuni za uendeshaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja
na mamlaka ya kutenga maeneo ya biashara na kuwaruhusu wale wanakidhi masharti
ya leseni zao kufanya biashara zao ila wengi wao hasa madereva wa Bajaji na
Bodaboda hawazingatii haya” Amesisitiza Mh. Sadiki.
Ameeleza
kuwa sheria zote zilizotungwa zimewekwa ili zifuatwe kwa ustawi wa taifa na si
vinginevyo na kubainisha kuwa wote waliovamia maeneo ya vituo vya mabasi,
maeneo ya vituo vya umeme na hifadhi za barabara ni vema wakaondoka wenyewe na
kukubali kutii sheria bila shuruti huku akitoa mfano wa baadhi ya
wafanyabiashara na wauza vyakula “mama lishe” walio anza kuvamia maeneo ya
ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo Kasi (DART).
“Haiwezekani
sheria za jiji zikavunjwa na sisi tukaendelea kuwaangalia baadhi yao wamefikia
hatua ya kuvamia maeneo ya mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuanza kufanya
biashara na kuwasumbua mafundi jambo lisilokubalika”
Akizungumza
kuhusu biashara ya bodaboda inayofanywa na vijana walio wengi jijini Dar es
salaam Mh. Sadiki ameeleza kuwa mpango wa serikali kuruhusu Bodaboda na Bajaji
kutumika kubebea abiria ulikuwa na maana nzuri ya kuwawezesha wananchi kupata
usafiri hasa katika maeneo yasiyofikika kirahisi kwa magari hasa vijijini na
kuongeza kuwa utakua na mafanikio kama watafuata sheria.
‘Serikali
iliruhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji kutumika kubebea abiria kwa nia nzuri
ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafiri na kuongeza ajira,hivyo siyo nia yetu
kuwadhalilisha vijana hawa tunachowataka wafanye ni kufuata sheria za nchi”
Aidha
kwa upande wa ongezeko la ombaomba ambao baadhi yao walirudishwa katika maeneo yao
ya awali na kurejea tena jijini Dar es salaam ameeleza kuwa utaratibu wa
kuwafuatilia uko pale pale na kufafanua kuwa watakaokutwa na makosa ya kukaa
maeneo yasiyoruhusiwa watafikishwa mahakamani.
Kwa
upande wake Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna (CP) Suleiman
Kova ameeleza kuwa ni wakati sasa wa wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan
madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria na kusisitiza kuwa ni vema
wananchi wakajenga mazoea ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo
vya kuwawezesha kutembea barabarani.
“Kwa
waendesha pikipiki “bodaboda” hali ni mbaya wengi wameumia na kupata ulemavu wa
kudumu kwa kutozingatia sheria za usalama barabarani na kukidhi matakwa
ya kuendesha pikipiki hizo”
Amesema
kuwa Jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa kushirikiana na manispaa zote tatu
kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa sheria vinakomeshwa na kutoa wito kwa
wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona dalili zozote za uvunjifu wa amani hasa
matukio ya ujambazi kwa kutumia pikipiki yayoendelea kuongezeka kwa kasi.
“Napenda
niwahakikishie wananchi kuwa jeshi la polisi tumejipanga vizuri kukabiliana na
vitendo vyote vya uhalifu wa aina zote, pia natoa wito kwa wakazi wa jiji la
Dar es salaam hasa wafanyabiashara kuepuka kutembea na fedha nyingi ili kuepuka
madhara ya kuvamiwa”
Naye
Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio ameeleza kuwa
sheria ya usafirishaji kusimamia Bajaji na Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa
serikali ina wajibu wake na pia waendesha pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa
kuzingatia kanuni taratibu na kanuni zilizowekwa.
“Sisi
kama SUMATRA tunaendelea kufanya kila tuwezalo kukabiliana na vitendo vyote vya
uvunjivu wa sheria za barabarani”

