Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Wekundu wa Msimbazi
Simba wametamba kupambana hadi dakika ya mwisho mbele ya Azam FC katika mchezo
wa nusu fainali ya kombe la shirikisho utakaochezwa kesho kwenye uwanja wa
taifa jijini Dar es salaam.
Mratibu wa Simba, Abbas Ally amezungumza na The Capitaltz.com kuhusu
maandalizi na matarajio ya kikosi chao ambacho kiliweka kambi ya siku tano
mjini Morogoro kwa ajili ya kujiwiwnda na mchezo huo.
Abbas amesema wamejiandaa vyema kuwakabili Azam FC na wana
matarajio makubwa ya kupambana vilivyo ili kuhitimisha lengo la kuibuka na
ushindi, ambao pia utakua ni sehemu ya kulipiza kisasi cha kufungwa na wana
Lambalamba hao katika mchezo wa ligi pamoja na kombe la Mapinduzi mapema mwaka
huu.
Kwa upande wa Azam FC, mapema hii leo afisa habari wa mabingwa
hao wa Afrika mashariki na kati Jaffary Iddy Maganga alizungumza
na waandishi wa habari kwa ajili ya kuelezea maandaliazi ya kikosi chao ambacho
kimedhamria kutoipoteza nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kombe la
shirikisho barani Afrika mwaka 2018.
Jaffary Iddy amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri baada ya
kufanya maandalizi ya kutosha kwa kipindi cha siku kadhaa, sambamba na kucheza
mchezo wa kirafdiki dhidi ya African Lyon juma lililopita.
Hata hivyo Jaffary Iddy amesema pamoja na kuwa na mwenendo mzuri
dhidi ya Simba tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2017, bado kesho watakwenda uwanja
wa taifa wakiwa na tahadhari kubwa kwa kufahamu, mnyama atakua amejiuliza kwa
nini alipoteza mara mbili dhidi yao.