Simba na Yanga watakutana Jumanne Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
Hiyo inafuatia Simba SC kushinda 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys jioni ya jana katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan.
Matokeo hayo yanaifanya Simba imalize kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Jang’ombe Boys, Taifa jang’ombe zenye pointi sita kila moja na URA yenye pointi nne.
Ikumbukwe Yanga imeshika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya Azam walioongoza kwa wastani wa mabao baada ya kufungana kwa pinti saba kila timu.
Katika mchezo wa jana, mabao yote ya Simba SC yamefungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo moja kila kipindi.
Mavugo aliyesajiliwa Simba SC msimu huu kutoka Vital’O ya kwao Burundi, alifunga bao la kwanza dakika ya 11 kwa shuti baada ya kuukuta mpira uliorudi baada ya kuogonga nguzo ya lango kufuatia shuti la winga Shiza Kichuya aliyepokea pasi nzuri ya mshambuliaji mzawa Juma Luizio.
Mavugo akafunga bao la pili dakika ya 53 kwa shuti kali tena baada ya kupokea pasi ya Kichuya pembeni kulia na kumkokota beki wa Jang’ombe hadi kwenye 18 kabla ya kufunga.
Bao hilo likawafanya Jang’ombe Boys wapoteane na kuwapa fursa Simba SC walio chini ya kocha
Mcameroon, Joseph Marius Omog kutawala zaidi mchezo.
Kilichofuatia ni kasi ya mashmbulizi mfululizo langoni mwa Jang’ombe Boys na kosa kosa za mabao ya wazi hadi filimbi ya mwisho. Baada ya mchezo huo, Mavugo akachaguliwa kuwa mchezaji bora.
Nahodha Jonas Mkude akasema wamefurahi kwa ushindi huo na kuongoza Kundi A na kwamba kuelekea mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya mahasimu, Yanga hawana wasiwasi.
“Sisi tumejiandaa vizuri, ni matumaini yetu na wao wamejiandaa vizuri, mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi, baada ya maandalizi tutakutana tutacheza, utakuwa mchezo mzuri, kipimo kizuri kwetu na kwao, dakika 90 zitaamua,”.
Siku hiyo pia jumanne nusu fainali ya kwanza itakuwa Taifa Jang'ombe dhidi ya Azam Fc itakayochezwa saa 10:00 jioni