TUNDA LA HAYATI DK MVUNGI KWA WATANZANIA - CAPITAL TZ BLOG DODOMA

Latest

BANNER 728X90

Sunday, 16 February 2014

TUNDA LA HAYATI DK MVUNGI KWA WATANZANIA

Dk Natunjwa Edmund Adrian Sengondo Mvungi, ni mzaliwa wa kwanza wa aliyekuwa kingunge wa sheria, Dk Sengondo Mvungi (61) ambaye Oktoba 12, mwaka jana alivamiwa nyumbani kwake na kujeruhiwa kabla ya kufariki dunia akiwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.

Natujwa ni daktari katika taaluma ya sheria, Mkufunzi na Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo, kilichopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Daktari huyu wa sheria ni miongoni mwa wateule 201 wa Rais Jakaya Kikwete, wanaotarajiwa kuungana na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuunda Bunge Maalumu la Katiba Mpya.

Kwa fursa hiyo, atashiriki kuboresha Rasimu ya pili iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo hayati Dk Mvungi, (baba yake) aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, mpaka anapatwa na tukio lililosababisha kifo chake, alikuwa katika hatua za mwisho za kushirikiana na wajumbe wenzake kuandika rasimu hiyo ambayo iliwasilishwa kwa Rais, Desemba 30, 2013.

Katika mahojiano maalumu Dk Natujwa Mvungi, anasema nafasi ya kuwakilisha Taasisi za Elimu katika bunge hilo, ameipata baada kupeleka jina na taarifa muhimu zilizotakiwa kuelezea sifa zake zikiwamo za taaluma na kwamba anaamini uteuzi huo wa Rais umemtendea haki ambayo anastahili.

“Naamini nimeteuliwa kutokana na kuwa na vigezo vilivyohitajika; nilipeleka jina na maelezo ya sifa zangu, nashukuru nikateuliwa natarajia kuwa wajumbe sote tutatekeleza jukumu lililo mbele yetu kwa kuzingatia mifano ambayo tayari imeoneshwa na viongozi mbalimbali, kupitia mijadala inayoendelea ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba,” anaeleza.

Dk Natugwa mwenye umri wa miaka 32, anaamini kupevuka kwake kitaaluma na kiwango chake cha kuifahamu jamii ya Watanzania, vikikolezwa na malezi mazuri aliyopewa na wazazi wake, atamudu kuwakilisha siyo tu kundi la jamii lililompa nafasi ya kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba, bali Watanzania kwa ujumla.

Anasema pamoja na masuala ya elimu kuwekwa katika eneo la haki za binadamu ndani ya rasimu ya Katiba mpya, anaamini eneo hilo bado linahitaji kuboreshwa zaidi kwa kuzingatia kuwa Katiba hiyo ni ya Jamhuri ya Muungano na elimu siyo moja ya mambo ya muungano.

Anabainisha anavyovutiwa na ukomavu wa kizalendo unaoendelea kuonekana miongoni mwa wanasiasa na viongozi wastaafu nchini, anawataja Jaji Joseph Warioba, Profesa Phillemon Sarungi na Joseph Butiku.

“Hata unapofuatilia wanavyojadili masuala ya Katiba mpya, unabaini walivyokomaa kizalendo wanafaa kuigwa na sote tutakaojadili rasimu ya pili ili kutoa Katiba inayopendekezwa, kazi hii ndiyo kitovu cha utaifa wetu; siyo siri wameonesha mwanga ambao tukiufuata tutaandika historia ya uzalendo duniani,” anaeleza Dk Natujwa

Mwananchi Jumapili: Una mpango wa kuwa mwanasiasa?

Dk Natujwa: Sina jibu la moja kwa moja. Kwa sababu siasa ni maisha ya kila siku, mfano: kukitokea mgao wa umeme nikafuatilia ili nijulishwe tatizo, nikashiriki kutafuta ufumbuzi tayari nakuwa mwanasiasa. Kwa maana hiyo, hata sasa mimi ni mwanasiasa.

SOURCE: MWANANCHI