MKUU WA
MKOA WA DODOMA MHE. JORDAN RUGIMBANA
AELEZEA AZMA YAKE YA KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA KUPITIA SHUGHULI ZA
UZALISHAJI MALI WAKATI ALIPOKUTANA NA BALOZI WA USWISI NCHINI TANZANIA
(Na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma)
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana amemuomba balozi wa Uswisi
hapa nchini Mhe. Florence Tinguely Mattli kusaidia kuunga Mkono jitihada za
Serikali ya Mkoa wa Dodoma za kuongeza ajira kwa vijana kupitia shughuli za
uzalishaji mali na utoaji huduma mbalimbali.
Mhe. Rugimbana alimweleza balozi
wa uswisi hapa nchini kuwa moja kati ya vipaumbele vyake kwenye Mkoa wa Dodoma
ni kuzalisha ajira kwa vijana kupitia uundaji wa makambi ya vijana ya
uzalishaji mali na shughuli za kiuchumi kupitia sekta za kilimo, ufugaji na
utoaji huduma mbalimbali, jambo ambalo hata viongozi wakuu wa kitaifa wamekuwa
wakisisitiza.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
alipokutana na balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattli na ujumbe wake
wakati walipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali
ya maendeleo hapa Mkoani Dodoma na miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali
ya Uswisi
Katika kufanikisha azma hiyo Mhe.
Rugimbana alisema kuwa serikali ya Mkoa wa Dodoma imejipanga kutoa ushirikiano
wa hali ya juu kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wanaofadhili miradi ya huduma
za jamii na uzalishaji mali, na kuongeza kuwa kwa sasa serikali ya awamu ya
tano imejikita katika kutaka wananchi kufanya kazi hususani vijana kuachana na mambo
ambayo yanawapotezea muda bure kama michezo ya ‘pool’ badala yake wajikite kwenye
shughuli za uzalishaji mali, lakini pia serikali inajukumu la kuwajengea vijana
mazingira mazuri ya kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake balozi wa Uswisi
hapa nchini Mhe. Florence Tinguely Mattli amemwambia Mhe. Rugimbana kuwa Nchi
yake ya Uswisi na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa karibu wa muda mrefu na
imekua ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za jamii. Aliongeza
kuwa katika ushirikiano huo Mkoa wa Dodoma ni moja kati ya Mikoa waliyoipa
kipaumbele.
Alisema nchi yake inaunga Mkono
jitihada za serikali za kuongeza ajira kwa vijana kupitia mradi wa Kuongeza
Fursa za Ajira kwa Vijana kupitia shughuli za uzalishaji mali za
kilimo, mifugo na usafi wa mazingira ambao unawalenga vijana wenye umri kati ya
miaka 18 hadi 30 ambao hawana ajira, wale ambao hawakupata nafasi za kupata
elimu na wale walio vijijini na hususani wale wenye malengo ya kupata ajira au
kujiajiri kupitia fursa mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao.
Mradi huu unafadhiliwa na
kutekelezwa na shirika la maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) kwa
kushirikisha wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika la kimataifa la
maendeleo la Uholanzi (SNV) ambapo awamu ya kwanza itaanza 2016 hadi 2018 na
utajumuisha mikoa ya ukanda wa kati ikijumuisha Dodoma, Singida, Tabora,
Shinyanga na pia Morogoro kwa mwaka wa 2016 pekee umetengewa jumla ya Euro 1.4
Milioni
Balozi Florence Tinguely Mattli
aliongeza kuwa mradi huo utahusu kuwawezesha vijana eneo la utaalamu na mafunzo
ya ufundi na stadi za maisha, na pia uwezeshaji wa uanzishaji miradi ya
uzalishaji mali baada ya mafunzo. Alisema kupitia miradi ya uzalishaji
kwenye kilimo, ufugaji nishati na usafi
na utunzaji Mazingira, vijana wataboresha hali za maisha yao na kujipatia ajira
na kipato.
Alisema changamoto inayoikabili
sekta ya ajira kwa vijana ni pamoja na mtazamo hasi na imani haba juu ya uwezo
na utaalamu wa vijana hasa upande wa waajiri wa sekta binafsi, lakini pia sekta
za uzalishaji mali alizozitaja hapo juu bado hazijaweza kutoa mchango
unaoridhisha kwa Taifa, wakati zinafursa nyingi za kuzalisha ajira kwa vijana
na kuchangia pato la taifa.