Vijana 11 waliokuwa na shauku ya kujiunga na Chuo cha Polisi Moshi (MPA) wamejikuta wakitapeliwa kati ya Sh. milioni moja hadi milioni 1.5 kila mmoja, baada ya kulaghaiwa na mmoja wa askari mgambo mjini humo kuwa atawapatia nafasi ya kujiunga na chuo hicho.
Habari za uhakika zilizopatikana mjini hapa jana na baadae kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa na Mkuu wa chuo hicho, Kamishna Mwandamizi Matanga Mbushi, zinaeleza kwamba, vijana waliotapeliwa wanatokea mkoa wa Mbeya.
Kamanda Mutafungwa alisema jana kwamba, Jeshi la Polisi halijatangaza nafasi za mafunzo hayo na kwamba mtuhumiwa aliyefanya utapeli huo ambaye ni askari mgambo mkazi wa Mbeya, amekamatwa mjini Moshi na anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Tunamshikilia mgambo huyo katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kumuhoji na tutamsafirisha jijini Mbeya kwenda kujibu mahakamani tuhuma zinazomkabili. Hawa vijana walipohojiwa walisema walichukuliwa eneo la Mbalizi, Mbeya,” alisema.
Kufuatia tukio hilo, polisi mkoani Kilimanjaro wamelazimika kutafuta mawasiliano ya wazazi wa vijana hao kwa ajili ya kutuma fedha za nauli za kuwasafirisha kurudi nyumbani hadi hapo kesi ya msingi itakapofunguliwa jijini Mbeya.
Wakati vijana hao wanakamatwa katika chuo hicho, walikuwa wamefungashiwa vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kujiunga na Jeshi la Polisi.
Alipotafutwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi, Mbushi ili kuzungumzia suala hilo, alisema katika uchunguzi wao wa awali wamebaini kwamba kuna askari mmoja mwenye cheo cha koplo kutoka mkoa wa Mbeya alihusika na alichukua fedha hizo lakini hakuja Kilimanjaro.
Alisema mgambo huyo alikamatwa baada ya kufika chuoni hapo akiwa ameambata na vijana hao 11, wavulana wanane na wasichana watatu.
Aliwataka wazazi kuelewa kwamba, nafasi za mafunzo ya polisi hazinunuliwi na wala haziuzwi mitaani, bali muda unapofika huwa zinatangazwa na kuwataka zinapotangazwa nafasi hizo waende wakaulize kwenye ofisi za wakuu wa polisi wa mikoa na wilaya ili waweze kupata uhakika na kujulishwa hatua wanazotakiwa kuzifuata ili kukidhi vigezo vya kujiunga na Jeshi la Polisi.
Hili ni tukio la pili la vijana kutapeliwa fedha wakilaghaiwa kutafutiwa nafasi za kujiunga na mafunzo ya polisi, la kwanza likiwa ni 2015 vijana 90 kutoka jijini Dar es Salaam walipotapeliwa kwa njia hiyo.