ALIYEKUWA Askofu wa Jimbo Kuu la Dodoma la Kanisa Katoliki, Mathias Isuja (87) amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar Itigi mkoani Singida.
Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga, alisema askofu huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Alisema alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tumbo.
“Tumepata msiba Jimbo Kuu la Dodoma kutokana na kifo cha Mhashamu Askofu mstaafu Mathias Isuja. Kifo kimetokea usiku wa kuamkia leo (jana) katika Hospitali ya Rufaa Itigi,”alisema Padre Chesco.
Alisema mazishi yatafanyika Jumatano ijayo jimboni hapo na tayari mwili wa marehemu umekwisha kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.
“Tunaomba waumini waendelee kushikamana katika kipindi hiki kigumu cha majonzi cha kuondokewa na Askofu wetu,”alisema.
Alisema mwaka jana Askofu Isuja alikwenda India kabla ya kurejea Tanzania na kuendelea na matibabu kutokana na ugonjwa huo wa saratani ya tumbo.
Isuja alizaliwa Agosti 14 mwaka 1929, Haubi wilayani Kondoa.
Alianza masomo yake ya ukasisi Desemba 24 mwaka 1960 na kupewa Daraja Takatifu la Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Dodoma.
Juni 26 mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma na kuwekwa wakfu Septemba 17 mwaka 1972 kabla ya kustaafu Januari 15 mwaka 2005.
Wakati huohuo, Rais Dk John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Askofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kutokana na kifo cha Askofu mstaafu Mathias Issuja.
Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema Askofu mstaafu Mathias Issuja alikuwa mzalendo wa kweli, kipenzi cha watu, aliyefanya kazi kubwa ya kuwajenga watu katika roho na mwili, na kamwe mchango wake katika maendeleo ya elimu, afya na malezi ya watoto yatima hautasahaulika.
“Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Baba Askofu Mathias Issuja. Kazi kubwa aliyoifanya duniani kuwahudumia watu kiroho na kimwili ni vigumu kuipima, nitamkumbuka daima,” alisema Rais Magufuli.