Dodoma. Wafanyabiashara wa simu za mkononi mkoani hapa wameiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) isizifungie simu feki kwa madai kuwa wanaziuza bila kujua viwango vyake vya ubora.
Wafanyabiashara hao walitoa ombi hilo ikiwa ni siku moja tangu TCRA itoe msimamo wake kuhusu kuzifungia simu hizo mjini hapa.
Hata hivyo, TCRA ilisema lazima simu hizo zizimwe ifikapo Juni, mwaka huu huku ikitoa rai kwa wenye mashaka na simu wanazotumia, wazirudishe kwenye maduka waliyonunua.
Kauli hiyo ilitolewa juzi kwenye semina ya wauzaji wa simu wa mjini Dodoma iliyoendeshwa na TCRA kwa lengo la kuwakumbusha muda wa kuzima simu hizona kuwataka wafanyabiashara wasiendelee kuziuza kwani wanaitia hasara Serikali na watumiaji wa simu.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Bakari Msangilwa alisema TCRA ikiamuru kufungwa kwa simu hizo watalazimika kufunga biashara ili kukwepa migogoro kati yao na wanunuzi sokoni. Msangilwa alisena hata wao wakati mwingine huziuza simu hizo bila kujua kama ni bandia au la. Mfanyabiashara mwingine, Shekifu Bakari alilitaka Shirika la Viwango nchini (TBS) kufunga stika kwa kila simu ili Watanzania wazitambue feki na zilizoruhusiwa ili kukwepa uchakachuaji.
Akijibu ombi hilo, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema taarifa kuhusu muda wa kuzifunga simu hizo ilitolewa na mamlaka hiyo muda mrefu, hivyo hawapaswi kuwa na visingizio.
Awali, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Francis Mwonga alisema bado kuna upotoshwaji kutoka kwa baadhi ya watu kuwa kazi hiyo ni danganya toto.
Mwonga aliitaka TCRA kulivalia njuga jambo hilo na wasimuonee mtu haya.