Naibu Waziri Ofisi Ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Selemani Jafo, amewatoa hofu wahitimu wa Kozi ya Ualimu ambao wamekuwa wakisubiri ajira kwa muda mrefu.
Akizungumza na Lindiyetu.com leo Jijini Dsm Naibu Waziri Jafo amewataka wahitimu hao kuwa na subira kwani ajira hizo zitatangazwa muda wowote kutoka hivi sasa, huku akiwahakikishia kuwa wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu wamejipanga kuhakiki idadi ya walimu wanaohitajika.
Ameongeza kuwa licha ya uhakiki huo pia wizara yake inamalizia takwimu za walimu waliostaafu kazi pamoja na waliohama kutoka shule binafsi ili serikali iweze kujua idadi halisi ya nafasi zinazoitajika.
Jafo ameiambia Lindiyetu kuwa mwaka huu serikali inampango wa kuongeza idadi ya ajira za Walimu hadi kufikia Walimu 40,000 katika ngazi za Shule za Msingi na Sekondari.
Kuhusu ajira hizo Jafo, amefafanua kuwa mikoa ya Kigoma, Mara, Tabora na Rukwa ndio itapewa kipaumbele kwani ndio inaongoza kwa kuwa na idadi ndogo ya Walimu na hii itapunguza kasumba ya wahitimu kozi ya ualimu kupenda kuajiriwa mjini.