Wakazi wa eneo la Zingiziwa Wilaya ya Ilala wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulifutia hatimiliki shamba la zaidi ya hekari 10 lililotengwa kwa ajili ya hifadhi ya wanyama (Zoo) kwa madai kuwa limejaa chatu ambao wamekuwa tishio kwa wananchi hao.
Wakazi hao walisema Manispaa ya Ilala ilitenga shamba hilo kwa ajili ya hifadhi tangu mwaka 2005 lakini mpaka sasa halijaendelezwa matokeo yake limekuwa kichaka cha kujifichia majambazi huku wananchi wakiumwa na nyoka hao.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Mohamed Kaunda alisema ni vizuri serikali ikachukua hatua kwani ilishaelekezwa kuwa mashamba makubwa yasiyoendelezwa yapokonywe na yarudishwe Serikalini kwa ajili ya kujenga huduma kwa jamii.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Ally Mkwanda alisema katika mtaa wake wapo watu wanamiliki hekari kuanzia tano hadi 10 wanashindwa kuyaendeza na kuyafanyia usafi matokeo yake eneo hilo linaonekana kuwa chafu na kumsababishia kushindwa kutekeleza agizo la Mkuu wa mkoa huo kuwa kila mtaa uwe safi.
“Kikwazo kikubwa katika mtaa wangu wamiliki wa maeneo wameyatelekeza, yamekuwa kichaka cha wezi na kuwa na nyoka wakubwa ambao ni hatari kwa wananchi wangu ambapo imenisababishia mtaa wangu kuonekana mchafu,alisema Mkwanda.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,Isaya Mgulumi alisema eneo la lipo kwenye mpango wa kuanzisha Zoo na pembeni watajenga viwanja vya michezo ili kuondoa hilo pori.
Alisema mpaka sasa sh100 milioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo na amewataka wananchi wa eneo hilo kuondoa hofu.
- See more at: http://edwinmoshi.blogspot.com/2016/04/chatu-wazua-kizaazaa-dar-es-salaam.html#sthash.WR5HVejs.dpuf