Na Baraka Mbolembole
Mangapi umeyaona ambayo hujayapenda? Kiasi inawaumiza, lakini njia ngumu wanayopitia mashabiki wa Simba SC hivi sasa iliandaliwa na baadhi ya wanachama na pengine kipigo cha jana Jumapili katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kimewafedhehesha sana kwani timu iliyowafunga (Toto Africans) ilianza na wachezaji ‘vijana’ watano waliosajiliwa msimu huu baada ya kutemwa na Simba.
Yanga SC wamekula vizuri ‘viporo’ vyao vyote na kukusanya alama 59 katika kiti cha uongozi baada ya kucheza michezo 24. Mchezo wa 25 kwa Simba ulikuwa mwepesi kupita kiasi, na mashabiki, wanachama, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi.
Lakini upande wangu niliwaambia ‘watapigwa’ na ‘vijana wao wenyewe’. Kweli, Simba imechapwa 1-0 na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili ya msimamo wakiwa na alama 57 huku wakitangulia game moja mbele.
Hakika inakatisha sana tamaa, inahuzunisha lakini upande mwingine natazama matokeo yao kwa misimu hii minne kama ‘fundisho lenye tahadhari’ kwa wanachama wa klabu ambao miaka ya karibuni kura zao wakati wa chaguzi kuu za klabu huwa zinakwenda kwa watu wasio na ufahamu na mambo ya soka.
Acha tu ‘Simba Yangu ipigwe,’ acha tuendelee kusotea mafanikio ya ndani ya nchi ambayo yalizoeleka ili watu wajifunze kuwa nyakati hizi ‘si kila mtu mwenye pesa anaweza kuwa kiongozi mzuri.’ Uongozi ni kipaji kinachoendana na taaluma ya mhusika.
Wakati Yanga ikipambana kimbinu, kiakili na kiufundi kushinda kila mchezo wao wa viporo (Yanga 2-1 Mwadui FC kisha Yanga 1-0 Mtibwa Sugar) katika uwanja wa Taifa. Yakaibuka maneno kwamba wanabebwa na waamuzi jambo ambalo si la kweli.
Simba wenyewe walichapwa 2-1 na kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya kombe la FA na timu ya Coastal Union, pia wamechapwa 1-0 na Toto katika VPL. Yaani, ‘chakula cha leoleo kinachacha!’
‘Simba wataendelea kupita ninapotaka wapite sababu hawana kipya.’ Kipigo cha Toto dhidi ya Simba ‘si habari’ na mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara ‘watapigwa’ tena na Azam FC katika mchezo ujao.
Kwanini mashabiki walihamaki na kuwarushia maneno makali baadhi ya viongozi wao wa juu ambao walikuwa jukwaa kuu? ‘Mafionso’ napenda kuwaita hivyo wataendelea kuwaliza, kwa sababu ni ninyi wenyewe mliokubali kuwatii.
YOTE HAYA YAMEANZIA HAPA
Tatizo la kwanza Simba lipo katika baadhi ya watu katika inayoitwa Kamati ya Usajili, pili kwa Rais wa klabu ambaye kwa hakika amekosa ‘meno’ hata ya kutafuna kitu laini labda tuseme tunda zuri la Embe, tatu ni wachezaji. Utawala wa sasa ulingia kwa sera ya ‘ pointi3’ unajua ilikuwa na maana gani? Utajua, baki nami hadi mwisho.
Kwa asilimia 100 nimekuwa nikipinga ‘kampeni’ ya baadhi ya Wana-Simba ambao wanashikilia msimamo wa kutaka kuona klabu hiyo inauzwa kwa bilionea, Mohamed Dewji ambaye yu tayari kuwekeza kiasi cha billion 20 huku akinunua hisa za asilimia 51 za umiliki wa klabu. Napinga kwa kuwa naamini Mo si suluhisho la kuifanya Simba kuwa klabu bora na yenye mafanikio Afrika.
Kuwekeza ni jambo moja, na mafanikio ni jambo lingine. Simba inaweza kuuzwa lakini si kwa namna ya kushinikiza kwa kuwa timu imekaa misimu mitatu bila kushinda chochote. Simba kwa sasa imekuwa ikiangushwa na utawala, ule wa Aden Rage ambao niliishia kukwaruzana nao mara kadhaa baada ya kuandika mara kwa mara kuhusu mwenendo na vyanzo vya migogoro.
Utawala uliopita, licha ya kuwa na ‘siasa nyingi’ uliweza kushinda taji la ligi kuu msimu wa 2011/12, pia timu ilifika hatua ya 16 Bora katika ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2011 (ilitolewa na kufika nane bora katika michuano ya Shirikisho)
Rage hakuwa na mafanikio makubwa lakini baada ya miezi 22 ya uwepo wake nje ya klabu hali inazidi kuwa mbaya zaidi licha ya utawala wa sasa kupigiwa sana debe wakati wa kampeni za uchaguzi.
Bahati mbaya, mashabiki wa klabu wamekuwa wanafiki, wale wanachama ambao walihakikisha baadhi ya wapambe wao wanashinda uchaguzi Juni, 2014 wamekuwa wa kwanza kuurushia makombora ya lawama utawala wa sasa.
Sasa wamekuwa wakisema, “Ni afadhali ya Rage” Kwa kipi kizuri ambacho Rage alikifanya? Kuwaita ‘Mbumbumbu!?’ Yaani mtu asiye na ufahamu wowote.
Rage aliitumia katiba ya Simba kumaliza muda wake wa miaka minne lakini ki ukweli ndiye mtu ambaye alipaswa kuondolewa Simba haraka hata kabla ya muda wake wa utawala kumalizika. Mara ya kwanza nazungumza na Rage ilikuwa baada ya kuandika makala.
“YUSUPH MANJI MTIHANI WA KWANZA KWA RAGE, SIMBA SC’. Makala haya niliandika Julai, 2012 katika gazeti la Dimba na nikaelezea namna Manji anavyoweza kufanikiwa na Simba kuanguka chini ya siasa za Rage.
Kwa Rage ilikuwa kosa, kwa wanachama/mashabiki wa Simba wakanirushia matusi mengi kama ilivyo kawaida yao. Miaka mitatu na nusu sasa ukweli wa makala ile umesimama Simba ‘wanasafa’, Yanga ‘wanaendelea kuchanua’.
YUSUPH MANJI NI MTU MAKINI KIUONGOZI, MATAJIRI WA SIMBA WAJIFUNZE
Manji ni mtu makini ambaye nilimuelezea kama atapata watu wazuri wa kufanya naye kazi Yanga itapata mafanikio. Mapema tu siku ile gazeti lilipotoka Rage akanipiga simu. “Utatuletea mgogoro” yalikuwa maneno yake ya kwanza kuniambia baada tu ya kujitambulisha kwa kuwa sikuwa na namba yake.
“Umesema mimi mtu wa porojo, si kweli. Kijana vitu vingine unapaswa kwanza kuniuliza kabla ya kuandika. Hivi unadhani Manji atanisumbua mimi? Labda Azam kwa kuwa ni timu ya mtu lakini si Manji. Yanga ni sawa na Simba tu, timu ya wanachama”, aliongea mfululizo licha ya awali kuwa na hofu baada ya kujitambulisha, nikajenga kujiamini baada ya kujua hakuwa mtu mwenye pointi za kunishinda.
“Samahani kiongozi, labda ni sehemu gani ambayo haikuwa sawa katika makala unisomee ili nijue kwa nini unalalamika?” nilimuuliza kwa kumtega, akaingia katika mtego wangu tukafungua dakika zaidi ya 20 za mazungumzo ambayo kwa hakika nilimkera sana, ila ndiyo ukweli unaoendelea sasa katika timu ya Simba.
“Wewe unasema Kelvin Yondan ni mchezaji huru una uhakika gani? Huyu ni mchezaji wetu halali na Yanga wamemsajili, nitahakika haki yetu inapatikana. Pia umesema kuwa mimi sijafanya chochote tangu niingie madarakani. Si kweli, nimerudisha umeme katika jengo la makao makuu ya klabu” Kabla hajaendelea kusema nikamkatiza.
“Lakini mimi sijazungumzia kuhusu ukarabati wa jengo bali nimezungumzia kuhusu ahadi kubwa iliyowafanya wanachama wakakupatia nafasi katika uchaguzi, nimezungumzia kuhusu ahadi yako ya uwanja wa klabu kabla hujamaliza muda wako. Muda unakwenda sasa na hakuna chochote kinachofanyika, au uliwadanganya wanachama wako?” nilimtupia swali hilo,
“Kijana, hata serikali ilitumia miaka 50 kujenga uwanja”, haraka alinijibu, “ Kwa hiyo ulidanganya?” nikamuuliza tena.
Sababu kubwa ya mazungumzo yangu na Rage ilikuwa ni kukosoa namna alivyochukulia usajili wa Kelvin Yondan kujiunga na Yanga. Mimi nilisema wazi Kelvin hakuwa na mkataba na Simba hivyo Yanga walikuwa sahihi kumsaini kwa sababu mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2011/12, Kelvin alikuwa huru tofauti na Rage aliyeshikilia msimamo kuwa mlinzi huyo wa kati alikuwa na mkataba wa miezi 6 mbele (kumbuka usajili wa Yondan kujiunga na Yanga, Julai, 2012 ulileta mvutano mkubwa sana.)
Wakati nakua nilikuwa shabiki mkubwa wa Rage-kiutawala, niliamini matatizo yote ya kiutawala katika FAT wakati huo yaliletwa na Muhidin Ndolanga, lakini kitendo cha kuwahadaa wanachama wake na kuwaambia Kelvin ni mchezaji halali wa Simba wakati tayari amejiunga na Yanga kilinifanya nijiulize mara mbilimbili.
Kama mtu niliyemjengea imani kubwa ya kiutawala, kama kiongozi bora katika soka kilikuwa sahihi. Rage alinivunja nguvu, kama kijana ambaye nimekuwa shabiki wa Simba kwa maisha yangu yote ya ufahamu, nikaanza kujiuliza, Je, mtu huyu anaweza kutimiza baadhi ya ahadi zake muhimu alizozitoa wakati anaomba kura ya kuiongoza klabu katika uchaguzi wa mwaka 2010?
Nilikuwa na imani kubwa kwamba chini yake Simba hata kama haitokuwa na uwanja wake wa mechi, ataiacha walau na sehemu nzuri ya makazi (hostel) na uwanja wa mazoezi, lakini hadi nilipoamua kuandika ‘YUSUPH MANJI MTIHANI WA KWANZA MKUBWA KWA RAGE, SIMBA SC’ Julai, 2012 nilijiridhisha kuwa hakuna chochote ambacho atakifanya zaidi ya ubingwa ambao Simba ilishinda Mei, 2012 katika mwaka wa pili wa utawala wa Rage klabuoi hapo.
Nakumbuka niliandika, “Kama Manji ataingia madarakani Yanga itamaliza katika nafasi waliyomaliza Simba msimu uliomalizika, na Simba wataangukia katika nafasi waliyomaliza Yanga msimu huu”.
Hapa nilikuwa nazungumzia endapo Manji angeshinda uchaguzi na kuwa mwenyekiti wa Yanga angeisaidia sana Yanga kushinda ubingwa msimu wa 2012/13 ubingwa ambao ulikuwa mikononi mwa Simba msimu ambao Yanga walimaliza katika nafasi ya tatu.
Nini kilichokuja kutokea?
“Kijana unaona (akanitajia mwandishi mmoja mkongwe wa michezo nchini) ananiandika mimi?” mazungumzo mengine kipande hiki daima yamebaki moyoni mwangu tu. Sijawahi kumwambia mtu na wala sitawahi kufanya hivyo, napenda kuwaheshimu watu na kuwapa hekima.
Kikubwa hapa, Mheshimiwa alishindwa kuipinga makala yangu hata wakati tulipokuwa tunazungumza. Ni kama mtu ambaye hakutaka kabisa wana-Simba waisome makala kama ile. Nakumbuka wachezaji wengi wa zamani walinipongeza nao wakaongeza uzito zaidi.
Nilikataa mwaliko usio rasmi wa kukutana na Rage lakini nilimwambia inaweza kutokea siku yeyote tukakutana. Nilitaka kuendelea kuiamini akili yangu tu. Kitendo cha kukataa kuonana naye naimani kilimfanya ajenge imani kwamba mimi ni mtu mwenye dharau.
Labda ni kweli, baadhi ya watu wengine wamekuwa wakisema pia mimi ni mtu mwenye dharau. Ukweli sikuona sababu ya kukutana naye kwa kuwa tayari aliniambia namna baadhi waandishi alionitajia walivyo upande wake na hivyo hawamsemi kwa ukweli.
SIMBA SI YAKO, SI YANGU, SI YAKE
Hii Simba si yako, si yangu, wala si ya yeyote. Mimi pia ni shabiki wa Simba lakini kwa miaka mitatu sasa wengi wamekuwa wakikataa na kunichukulia mimi ni ‘mnazi wa kutupwa wa Yanga SC.
Niwaambie ukweli tu kuwa ndani Yanga hakuna baya la kuliandika na unapotaka kuiandika Yanga hivi sasa kama huna pointi za mazuri yao utakuwa unakosea tu, Yanga hawana ubaya sasahivi ila nimewahi kukutana na vitisho vingi kutoka kwa wapenzi wa Yanga wakati nilipokuwa mstari wa mbele kuwashauri wamtimue, NCHUNGA mapema mwaka 2012.
Baada ya mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga kumshinikiza kocha, Papic kumpanga Nadir Haroub katika mechi muhimu dhidi ya Coastal Union licha ya kuambiwa mlinzi huyo wa kati alikuwa na adhabu ya kadi. Yanga ilinyang’anywa ushindi na kumaliza mbio zao za ubingwa ikiwa nafasi ya pili msimu wa 2011/12.
Nilikuwa nikiipinga sana system ya uongozi wa Nchunga nashukuru baada ya 5-0 Mei 7, niliwaambia Yanga watachapwa vibaya na Simba siku hiyo ili tu waamini kuwa Nchunga hakuwa mtu sahihi kuiongoza timu yao.
Kweli, wakapigwa mkono, nami nikasindikiza na makala ya kumtaka Nchunga ‘ajiuzulu kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa alijisifia mwezi mzima katika vyombo vya habari kwamba yeye ni kiboko wa Simba.
‘NCHUNGA, TAFAKARI KISHA CHUKUA HATUA…
‘Makala haya yaliwafanya hadi mashabiki wa Simba kunipongeza. Hadi kufikia sasa nimejifunza mambo mengi, unapoandika kitu cha kuikosoa Simba mashabiki wa timu hiyo watakwambia, “Wewe ni Yanga” na unapoandika baya kuhusu Yanga utaambiwa, ” Wewe ni Simba.”
Mimi nimekubali pande zote hizo kwa kuwa tayari nimetoka katika upenzi wa ‘Simba damu au Yanga damu’ mimi ni shabiki wa Simba, ila mpenzi wa mpira wa miguu. Unapokuwa na kiongozi mwenye ujasiri kama Rage na kushindwa kupata mafanikio tatizo ni nini?
‘SIMBA SC KATIKATI YA WANASIASA, ILA ITAVUKA’
Bonge moja la makala, pengine ndiyo makala yangu kali zaidi kuwahi kuiandika kuhusu Simba. Makala haya niandika Agosti, 2012 nakumbuka mwezi mmoja baadaye nilikwenda Morogoro kutazama mechi ya Mtibwa Sugar 3-0 Yanga SC, rafiki yangu wa muda mrefu, tulipokutana tu akaniambia, “Naomba twende nyumbani.” Nikakubali kwa kuwa hata kabla sijahamia Dar es Salaam tayari nilikuwa nimejenga mazoea ya kwenda kwao miaka na miaka kwani tulikuwa tukiishi mtaa mmoja. Ile kufika, moja kwa moja akanikaribisha ndani. Haraka akaenda katika moja ya vyumba, akarejea akiwa na baba yake.
Mzee Dogoli ni mtu anayenifahamu kwa kuwa kila asubuhi alikuwa anapita mbele ya barabara nyumbani kwetu, na nilikwisha jenga mazoea ya kumsalimia kiheshima. Nikampata heshima yake, akaitikia, kisha rafiki yangu akatamka, “Baba yule kijana aliyeandika makala ile ya Simba ndiye huyu hapa, humkumbuki?” Kwanza Mzee Dogoli (akiwa mkuu wa chuo cha habari mkoani Morogoro-MSJ) alionyesha mshangao wa wazi ambao niliushuhudia katika paji lake la uso, akaenda ndani. Kisha akarudi akiwa ameshika gazeti la Dimba, akalifungua hadi sehemu iliyokuwa na picha moja ya wastani akionekana Aden Rage, akaniuliza, “Ulifikiria nini kuandika makala haya?”
Kabla sijamjibu, akasema, “Nimesoma makala na habari nyingi za michezo kwa muda mrefu lakini hii ni bora kati ya zote, imenifumbua macho hata mimi baada ya kuisoma”.
KUMBUKA; Sikuandikii wewe, namuandikia yeyote yule akayeisoma hivyo msomaji wangu kuna mambo nitayagusa kwa kuwa nalenga nachokusudia, kuna watu watatajwa, lakini mwisho wa siku msomaji mwenyewe utapembua ili kujidhihirisha. Hii ni hoja tu, kumbuka katika hoja kweli huja…
Sababu kubwa ya kuandika makala yale, ‘SIMBA SC KATIKATI YA WANASIASA, ILA ITAVUKA’ ilikuwa ni baada ya wanachama wa klabu hiyo ‘kushindwa kisiasa’ katika jaribio lao la kutaka kumuondoa Rage madarakani na kujikuta wakiwashangilia ‘watawala’ wao mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa klabu mapema mwezi Agosti, 2012.
Niliwalaumu sana wanachama wa klabu, si kwa sababu yao kushindwa kumng’oa Rage madarakani bali kwa namna ‘walivyokubali kufanywa wajinga wa kufikiri.’ Ilinishangaza sana kuona, kusikia na kusoma katika vyombo vya habari jinsi walivyowasifia viongozi wao baada ya kuahidiwa kuwa matengenezo ya uwanja yataanza mara tu baada ya kupatikana ‘Hati ya Umiliki’ ya uwanja wao wa Bunju.
Nakumbuka, Rage alisema tatizo kubwa la kushindwa kuanza kwa ujenzi ni klabu kukosa milioni 30 ili waongezee katika kiasi kilichokuwepo ( mil.50) na kufikia milioni 80 ambazo zilihitajika ili kupatikana kwa hati hiyo. Wanachama waliingia katika mkutano wakiwa na jabza na walidhamilia kufanya mapinduzi ikiwa wasingepata maelezo yenye mwanga wa maendeleo siku za mbele.
Kumbuka, wakati mkutano huo unafanyika Rage alikuwa katika mwaka wake wa pili kama Mwenyekiti wa klabu, makamu wake alikuwa Geofrey Nyange Kaburu.
Kumbuka pia, ahadi kubwa ya Rage wakati wa uchaguzi wa klabu (2010) ilikuwa ni kuhakikisha anaiacha Simba ikiwa na uwanja wake wa kutumia, mechi na mazoezi. Hadi wakati wa mkutano (2012) hakuna kilichokuwa kimefanyika, zaidi ya mara kadhaa kusambaza picha ya ramani ya uwanja ambao utajengwa pale Bunju.
Rage pia aliingia katika mkutano akiwa na hofu na hadi kufikia siku ile nilikuwa nimeandika makala mbili kuhusu ‘taswira’ ya Simba katika siku za mbele kama tu ataendelea kuwa mwenyekiti wa klabu. Msimu wake wa kwanza katika ligi ya ndani ulimalizika kwa ‘fedheha’ hadi kwa wanachama na mashabiki baada ya timu kushindwa kutetea ubingwa wa ligi kuu.
Akirithi timu iliyomaliza msimu pasipo kupoteza mechi yoyote (2009/10) kutoka kwa utawala wa Mzee Hassan Dalali na mkufunzi ‘Simba Damu’ Mwina Kaduguda, Simba ilishindwa siku ya mwisho ya msimu na mahasimu wao Yanga (2010/11) katika mbio za ubingwa baada ya kuongoza ligi kwa zaidi ya alama 6 dhidi ya Yanga kuelekea mechi nne za mwisho wa msimu. Yanga ilishinda ubingwa kwa tofauti ya goli moja tu.
Baadhi ya wachezaji muhimu kama Musa Hassan Mgosi, Mohamed Banka, Uhuru Suleimani, Haruna Shamte, Salum Kanoni, Hillary Echessa, waliachwa baada ya kumalizika kwa msimu kwa sababu za ‘kufikirika’ kwamba walichangia timu hiyo kushindwa kutetea ubingwa wake.
Utawala wa Rage ulilia kuhujumiwa katika msimu ule, lakini ni wazi kuwa kiwango cha timu katika ligi ya mabingwa Afrika kiliwavutia wengi na hivyo ilichangia kushusha presha ya kushindwa katika ligi kuu Bara.
Simba ilifika 16 Bora ya ligi ya mabingwa Afrika licha ya kushindwa na TP Mazembe ndani ya uwanja. Simba ilikata rufaa na kushinda baada ya kugundulika kuwa TP Mazembe ilimtumia mchezaji asiyestahili kucheza. Rage alionekana kiongozi makini lakini ukweli ni ‘Mtu wa nje kabisa ya klabu aliyefanikisha hilo na si yeye.’
Kufungwa na Wydad Casablanca katika mechi ya 16 katikati ya 2011 kuliifanya Simba kuangukia katika michuano Shirikisho na licha ya kuanza na ushindi jijini Dar es Salaam, “Wekundu wa Msimbazi’ walipigwa 2-0 Kinshasa na Daring Club Motema Pembe ya DRC na ukawa mwisho wa timu hiyo katika michuano ya Afrika mwaka 2011.
Ni ajabu kuona ‘mwenendo mbaya’ wa Simba kwa misimu minne hii katika ligi ya ndani wakati ni timu ambayo ilishinda ubingwa bila kupoteza miaka mitano iliyopita huku ikifika walau hatua ya 16 bora katika michuano ya Ligi ya mabingwa na ile ya Shirikisho. Ubingwa wa Bara msimu wa 2011/12 ulikuja na kitu kikubwa-Ushindi wa 5-0 dhidi ya mahasimu wao Yanga, lakini kwanini timu ilikwenda chini haraka?
“Ninawashangaa wanachama wa Simba kushangilia kupatikana kwa million 30 za hati ya uwanja huku wakitangaza katika vyombo vya habari kuwa ni mchango wa haraka ambao ulipatikana mara tu baada ya Menyekiti wa klabu kusema kuwa tatizo linalochelewesha ujenzi wa uwanja ni hati.” niliandika hivi sehemu ya makala yangu ile, ‘SIMBA SC KATIKATI YA WANASIASA, ILA ITAVUKA’.
Kama unakumbukumbu, Simba ilikuwa imetoka kufanya biashara ya kwanza kubwa ya kuuza wachezaji wake Mbwana Samatta na Patrick Ochan kwa million 300 kwa klabu ya TP Mazembe miezi 11 nyuma.
Kwanza sikuridhishwa na aina ya sababu kuu iliyofanya kushindwa kuanza kwa ujenzi wa uwanja, pia kwa hakika kabisa sikukubaliana na wanachama wa klabu hiyo ambao walisema wamechanga haraka sana pesa za kufanikisha kupatikana kwa hati ya uwanja.
Rage ni mtu mwenye akili sana, pengine akili yake hufikiria kwa haraka sana pale anapokuwa katika wakati mgumu mbele za watu. Aliiendesha Simba kwa miaka minne kwa sababu tu aliweza ku-waendesha kwa ‘rimoti’ wanachama wake wote kwa vielelezo.
Ilikuwa ni asubuhi ya kama saa 2 hivi nilikuwa tayari nimekwisha pokea simu nyingi kutokana na makala niliyokuwa nimeandika. Mheshimiwa pia alinipigia simu muda huo nilioutaja. Kuna wakati niliacha kupokea simu kwa sababu nyingine zilikuwa za vitisho. Ni kati ya makala ambazo ziliwafumbua sana macho kuhusu ‘mwanasiasa’ waliyekuwa naye klabuni.
“Habari yako, mimi ni Aden Rage.” Nilisikia sauti ya upande wa pili katika simu ikinisalimu, tena ilikuwa na hofu, ilikuwa namba mpya katika simu yangu tena ni kati ya zile ambazo zilipigwa kati ya mara mbili hadi tatu lakini sikuzipokea. Kumbe alikuwa, Rage. Nikampa heshima yake, akaipokea kisha akasema, “Tayari nimepokea simu 19 kutoka kwa marafiki zangu, wote wananiuliza ‘Umeisoma makala ya leo? Je, unatatizo na huyu kijana aliyeandika?’ Labda na mimi nikuulize wewe, mimi nina tatizo na wewe?” Sikupindisha maneno, nikamjibu, “Hapana huna tatizo na mimi.” Akaendelea kuniuliza, “ Sasa kwa nini unaendelea kuandika?”
Kwanini niliandika makala ile, ‘SIMBA SC KATIKATI YA WANASIASA, ILA ITAVUKA’, KWANZA, Sikupendezwa na namna alivyowadanganya wanachama wa klabu yake kuhusiana na mkakati wa ujenzi wa uwanja.
Rage alisema tatizo ni milion 30 tu, jambo ambalo kwa nguvu nililipinga. Nilipinga si kwa nia mbaya, la!hasha, nilipinga kwa kuwa ndani ya siku 4 kuelekea siku ya mkutano mkuu wa klabu, uongozi wake ulitumia zaidi ya milion 60 kuwasaini wachezaji, Ramadhani Chombo na Mrisho Ngassa kutoka timu ya Azam FC.
Kipi kilifaa kuanza? Upande wangu, suala la uwanja lilipaswa kuwa kipaumbele cha kwanza na si usajili wa Chombo na Ngassa ambao Rage aliufanya ili kupunguza hasira za wanachama wao ambao hawakupendezwa na namna kiongozi huyo alivyochukulia suala la kushindwa kumbakisha Kelvin Yondan licha ya kuwaambia kuwa mlinzi huyo wa kati bado ni mchezaji halali wa Simba jambo ambalo halikuwa na ukweli.
“Samahani sana kwa kukutukana wakati ule ulipoandika makala yako kuhusu Manji na Rage (YUSUPH MANJI MTIHANI WA KWANZA KWA RAGE, SIMBA’, ulisema ipo siku Rage atalia kutokana na uwepo wa Manji, kweli nimemuona akilia, tena mbele ya wanahabari.”
Alinipigia siku moja mwanachama kiongozi wa juu wa matawi ya Simba jijini Dar es Salaam baada ya kushuhudia Rage akitoa machozi mbele ya waandishi wa habari mara baada ya Manji kubadilisha usajili wa Mbuyu Twite kutoka APR na kujiunga na Yanga SC, Agosti, 2012.
Niliwalaumu sana wanachama kushangilia upatikanaji wa milion 30 baada ya kupitishwa kwa ‘harambee’ kwangu haukuwa mchango wa wanachama bali ulikuwa mchango ‘bosheni’ uliofanywa na viongozi wa juu wa klabu.
Nakumbuka mwenyekiti wa klabu na makamu wake walichanga kiasi cha milion 5 kila mmoja (Rage na Geofrey Nyange Kaburu,) Zacharia Hans Poppe alichangia milion kumi, hao watatu tu ndani ya dakika 3 walichangia milion 20. Hawa si wote walikuwa ndani ya klabu kama watawala? Sasa kipi kilikuwa kinawafanya wanachama wa klabu kushangilia?
Rage alitumia siasa tu na akawashinda kirahisi lakini mimi sikuona ‘taswira nzuri mbele’ ndiyo maana niliendelea kumkosoa.
“Unaona unachoandika ni sahihi? Nimekuita, umeshindwa kuja na unaendelea kuandika” aliongea Rage mara baada ya kumjibu swali lake la kwanza ambalo aliniuliza kama yeye alikuwa na tatizo na mimi.
“Samahani sana kiongozi, unaweza kunisomea sehemu ambayo unaona haikuwa sawa katika makala yangu?” nilimuuliza swali la mtego ambalo liliendelea kumkwaza, sikujali, “Mimi nimezungumzia namna ulivyowahadaa wanachama wako katika suala la uwanja.”
“Kama milion 30 za hati ya uwanja zimekuwa kikwazo, je, uwanja utajengwa kwa pesa gani? Hiki ndicho nilichohoji, pia nimewalaumu wanachama kwa kukubali kudanganywa. Je, nimefanya kosa gani?” nilimwambia tena hata kabla hajanijibu.
“Naomba usiendelee kuandika, utatuletea mgogoro klabuni.” aliniambia Rage bila kunijibu wala kunisomea sehemu ambayo ilimfanya anipigie simu katika ile makala. Kuna vitu huwa sivijali sana, kutishwa ni jambo ambalo kamwe halijawahi kunisumbua na wakati huo nilipokuwa nazungumza naye nilikuwa na miaka 27.
Nilijiamini, “Nitaendelea kuandika kuhusu Simba kwa sababu mimi pia ni shabiki wa Simba tangu utoto wangu, sipendezwi na uelekeo wa timu.” nilimwambia. Kwa hasira akaniambia, “Mimi ni mtu mkubwa, naweza kufanya lolote, hivyo kama unaona unachofanya ni sahihi, sawa endelea kuandika.” Akaniambia.
“Naamini mtu mkubwa ni mwanafunzi, ambaye anapenda kujifunza zaidi na zaidi. Nakuhakikishia nitaendelea kuandika kuhusu Simba na kama mgogoro wowote utaibuka katika klabu ni sababu yako mwenyewe.”
Usikose hitimisho la makala haya siku ya kesho..
NB: Kwa ukaribu zaidi unaweza ku-LIKE Page yangu BSports tukajuzana mambo ya mpira kama hapa