SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi imekunjua makucha yake kwa kutangaza kuvifuta vyuo 10 ambavyo
havikusajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) .
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philip Mulugo, alitoa
kauli hiyo jijini Dar es Salaama mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na
kuongeza kuwa kufutwa kwa vyuo hivyo ni kutokana na kutokufuata utaratibu wa
kusajiliwa.
Alivitaja vyuo hivyo ni
Media and Research Center,
Vision Hotel and Tourism College,
East Africa College of Hospitality and
Tourism,
The Africa Institute of Business Management
Aspiration Training Center, vyote vya Dar es
Salaam.
Vingine ni Dar es Salaam School of Hair
Design,
Media and Values Training Institute na
Information Technology Training Center vya Dar es Salaam. Pia alikitaja Chuo
cha Morogoro School of Medical Sciences cha Morogoro.
Katika hatua nyingine, Mulugo alikiri kuwa kuna
upungufu katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia bodi ya
mikopo.
Alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili bodi
hiyo zikiwamo urejeshwaji wa mikopo kwa wanafunzi waliomaliza chuo, mfumo wa
utoaji wa mikopo, ufinyu wa bajeti na makosa yanayotokana na wanafunzi kukosea
kujaza fomu za mikopo.
SOURCE: MATUKIO NA VIJANA