
Waziri
huyo alikaririwa na gazeti hili akisema upo uwezekazo wa Katiba Mpya ya
Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ikiwa mchakato
wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakamilika kama inavyokusudiwa na
rasimu hiyo kupitishwa na wananchi katika ngazi zote bila mabadiliko.
“Watu
wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu itapita bila mabadiliko na
kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka Desemba inatosha kabisa kuandaa
Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na
Katiba Mpya,”alikaririwa akisema na kuongeza:
“Tunaweza
kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya Katiba lakini safari hii
tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee wakashiriki katika kuandaa
Katiba hiyo.”
Alisema
kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo inaweza isifanye kazi ya
kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama ilivyofanya sasa na badala yake
ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau kisha kupelekwa katika mabaraza
ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa
mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukamilika Aprili mwakani.
Alisema
kuanzia hapo, Serikali inaweza kuitumia tume ya sasa kutangaza rasimu ya
kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa kurejea maoni iliyokusanya hivyo
hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa rasimu hiyo kwenye mabaraza ya
Katiba kwa miezi miwili na baadaye kupelekwa katika Bunge la Katiba
jambo litakaloifanya ipatikane mapema.